Jumatatu , 9th Sep , 2024

Mama lishe wanaouza chakula kwenye mitaa mbali mbali jijini Dar es Salaam, wameomba Serikali iweze kuwajengea vibanda kwa ajili ya kujikinga na mvua ambazo zimekuwa zikipelekea kukosa wateja kwa maana hawana sehemu ya kujikinga.

Bahati Juma, mama lishe

Wakiongea na EATV, wanasema kipindi cha mvua hali huwa mbaya zaidi kwani wanakosa wateja kwa sababu hawana miundombinu ya kuruhusu wateja kutolowana.
“Kama wiki hizi mbili mvua zinanyesha kwahiyo tunakosa wateja kwa sababu wakija wanalowana inawalazimu wakale sehemu nyingine wakati sisi hapa tupo”, Bahati Juma, Mama lishe.
“Kama sasa hivi tunakosa wateja tunaomba Serikali au wadau watusaidie kutuwekea hata mabanda ya muda mfupi ili na sisi tuweze kujiingizia kipato maana tunategemea biashara hii kuendesha maisha yetu na familia zetu”, Rachel Maser, Mama lishe.
“Kuna siku nimeagiza chakula Hali ya hewa ikabadilika ghafla mvua ikashuka nimejibanza kwenye mti mimi nalowa, chakula kinalowa kwahiyo ni changamoto wakiwezeshwa tutakuwa tunastilika hapa”,Shaibu Yahya, Mteja.

Kutokana na changamoto hiyo Kampuni ya usafirishaji mizigo ya GTC, ikaona umuhimu wa kuwawezesha viti, meza pamoja na maturubai ya kisasa kwa ajili ya kuendesha biashara zao bila changamoto.
“Kutokana na changamoto wanazopitia hawa wakina mama tuliona kuna haja ya sisi kuwaunga mkono wakina mama hawa kwa maana kazi zetu zinategemea ili wao wakifanikiwa basi jamii nzima imefanikiwa, ndio maana tumewasaidia viti pamoja na matenti ya kujifunika na changamoto za Hali ya hewa”, Yassir Matsawiliy, Meneja mkazi GTC-Tanzania.