Jitihada za Tanzania za kusaidia kuleta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa katika nchi ya Sudani Kusini kwa njia mazungumzo umeanza kuonesha mwelekeo wa mafanikio baada ya viongozi wa makundi matatu yaliyotofautiana ndani ya chama cha (SPLM) kusaini makubaliano ya kusitisha mapigano na kuanza mazungumzo .
Wakizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo mbele ya marais Uhuru Kenyetta wa Kenya , Yoweri Museven wa Uganda na mwenyeji wao Rais Jakaya Kikwete, viongozi wa makundi yote yaliyotofautiana wameahidi kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa .
Kwa upande wao Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda wamewataka viongozi wa makundi hayo kuona umuhimu wa kutanguliza mbele maslahi ya wananchi wao wanaoendelea kuteseka kwa sababu ya tofauti za mitazamo ambazo zinaweza kumalizika bila kupigana , na wameipongeza Tanzania kwa kuendeleza harakati za hayati baba wa taifa mwalim Nyerere za kumaliza matatizo kwa njia za mazunguzo.
Awali mwenyekiti wa mazungumzo hayo John Malecela na katibu wa CCM iliyokuwa inaratibu zoezi hilo Abdulrahaman Kinana pamoja na kueleza baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa na pande zote likiwemo la kuheshimu uhuru na haki kila mwanachama kugombea nafasi za uongozi, wamewataka viongozi hao kuwa na uvumilivu wa kisiasa.
Akihitimisha kikao hicho Pais wa Tanzania Dkt Rakaya Kikwete amesema Tanzania itaendelea kutoa mchango wake wa hali na mali wa kupigania amani na kuhakikisha mazungumzo yanatumika kumaliza tofauti popote zinapojitokeza kwa kuwa ni jambo linalowezekana.
Zoezi la kuhitmisha makubaliano hayo kwa kutiliana sahihi lilitarajiwa kufanyika saa nne hadi saa tano mchana wa tarehe jana lakini halikuwezekana kutokana na kuibuka kwa mvutano miongoni mwao ambao ulisababisha zoezi hilo kumalizika saa Sita na robo usiku .