Alhamisi , 21st Dec , 2023

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Paul Makonda, amewatumia salamu watendaji wa Shirika la Umeme nchini TANESCO na kuwahoji kama wanatosha kuwa wawakilishi wazuri wa Rais Samia kutokana na malalamiko ya tatizo la kukatika umeme mara kwa mara 

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Paul Makonda

Makonda ametoa kauli hiyo leo Desemba 21, 2023, jijini Dar es Salaam, na kusema ni kweli changamoto ya umeme ipo lakini amedai kwamba huenda nyingine inasababishwa na uzembe wa watendaji.

"Chama kinataka kipeleke salamu kwa TANESCO je maumivu na mzigo na uchungu na shauku anayoibeba Rais Samia kuhakikisha tatizo la umeme linakuwa historia ndiyo hayohayo na watendaji wa TANESCO mmebeba?, ukiona Rais anafanya mabadiliko maana yake anafika hatua anasema hii haivumiliki, swali letu kwa TANESCO kweli mlipokaa na kilio na kelele za Watanzania juu ya umeme nyinyi mnajisikia fahari?, mnaona mnastahili kweli?" amehoji Makonda

Aidha Makonda ameongeza kuwa, "Mtendaji anatoa maelezo kwamba zile mvua zinazonyesha maji hayapiti huku halafu amekaa ofisini, katuonyeshee kule site, wananchi waone unachokisema ndiyo chenyewe?, pamoja na maelekezo yanayotolewa, chama kinaiuliza TANESCO mnaona mnafaa kumwakilisha Rais Samia?, kama leo Watanzania wakipiga kura sekta yenu ingepata asilimia ngapi za kutuongezea ushindi CCM?, wameahidi Januari kinu cha kwanza kinaanza kufanya kazi, ni matarajio yetu ahadi waliyoitoa iwe ni thabiti, hakuna kulala, hakuna kulipana posho, tunataka umeme,".