Jumamosi , 2nd Mei , 2020

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu, leo Mei 2,2020, ataongoza mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt Augustine Mahiga, aliyefariki mapema jana Mei 1, Jijini Dodoma baada ya kuugua ghafla.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu.

Mazishi ya Balozi Dkt Mahiga, yatafanyika mkoani Iringa katika eneo la Tosamaganga alikozaliwa huko Agosti 28, 1945.

Taarifa za kifo cha Balozi Dkt Mahiga, zilitolewa siku ya jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, na kueleza kuwa aliugua ghafla na mauti yalimfika njiani wakati akikimbizwa hospitalini.

Balozi Mahiga ni Mwanadiplomasia pia amehudumu katika nafasi mbalimbali, ikiwemo kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Kiongozi Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi, Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwa Umoja wa Mataifa na kama Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN) na Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Umoja wa Mataifa kutoka Somalia 2010 hadi 2013.