
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea mfano wa hundi kutoka kwa balozi wa Kuwait
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo leo Balozi wa Kuwait nchini Tanzania, Bw. Jasem Al-Najem amesema msaada huo ni mchango kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Makampuni ya Fouad Alghanim, Bw. Fouad Alghanim aishiye Kuwait.
Amesema watu kadhaa wameguswa na maafa yalitokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu na wameamua kuchangia ili kuisaidia juhudi za Serikali kukabiliana na hali hiyo ambayo haikutarajiwa.
“Tunatambua kuwa kazi ya kurejesha huduma kwa wananchi ni kubwa, na Serikali peke yake haiwezi kubeba mzigo wa kukarabati miundombinu na majengo ya ofisi na makazi ili kuurejesha mkoa huo katika hali yale ya kawaida,” amesema.
Akizungumza na Balozi Al-Najem ofisini kwake Bungeni, mjini Dodoma, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Tanzania imeguswa na moyo wa upendo kutoka kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Makampuni ya Fouad Alghanim na wenzake. Akitoa shukrani kwa msaada huo, Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali itahakikisha mchango huo unafikishwa Kagera kwa walengwa.