Jumatano , 6th Apr , 2022

Kufuatia kuanza kutumika kwa bei mpya za mafuta nchini Tanzania, leo Aprili 6/2022 Serikali imewaondoa hofu wananchi kuhusu upatikanaji wa nishati hiyo muhimu kwa kusema Mafuta yaliyopo nchini na yanayoendelea kushushwa bandarini yanatosheleza uhitaji wa mafuta nchini.

Waziri wa Nishati Januari Makamba akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 6/2022 Jijini Dar es salaam kuhusu upatikanaji wa mafuta Tanzania

Makamba akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam amebainisha kuwa kwa sasa kwenye maghala ya mafuta kuna hifadhi ya Lita Milioni 119 za petroli zinazotosheleza mahitaji ya siku 27, Dizeli zipo lita Milioni 116 na Mafuta ya taa zipo lita Milioni 6.8.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) jana ilitangaza kuanza kutumika kwa bei mpya ya nishati hiyo ambapo kwa sasa Petroli itakuwa 2,861 kwa lita, Dizeli 2,692 na Mafuta ya taa 2,682 kwa lita.

Ongezeko hili la bei linatajwa kusababishwa na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia kunakosababishwa na mapigano yanayoendelea baina ya Urusi na Ukraine ambao ni wasambazaji wakubwa wa nishati hiyo duniani