Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla
Badala yake Makalla ameuagiza uongozi wa Kijiji hicho,kata na Wilaya kutafuta eneo jingine kwaajili ya kujenga zahanati hiyo itakayowezesha wakazi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani kupata huduma za afya jirani.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa tamko la kupinga ujenzi wa Zahanati kwenye eneo la jirani na lilipo ghala na ofisi za kata ya Mpuguso alipozungumza na wakazi wa kijiji cha Kiwira jana kwenye mkutano wa hadhara ulioonekana kubeba hisia za watu wengi.
Makalla amekubaliana na baadhi ya wakazi wa kata hiyo waliosema mvutano uliozuka baina yao juu ya wapi zahanati ijengwe inatokana tu na tofauti za kisiasa ambapo baadhi ya wanasiasa wanataka kuutumia mgogoro huo kujinufaisha kisiasa.
Awali baadhi ya wakazi walisema kumekuwa na mgongano na mabishano baina yao kutokana na kile kilichoelezwa kuwa zipo tofauti za kisiasa baina ya uongozi wa kijiji cha Kiwira na ule wa kata ya Mapogoro.
Wamesema wakati mwenyekiti wa kijiji hicho anatokana na Chama cha Chadema,Diwani wa kata anatokana na Chama Cha Mapinduzi(CCM) hivyo kila upande umekuwa ukipendekeza sehemu yake ili kujenga Zahanati ya kijiji.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wamesema wanachohitaji wao ni kujengwa kwa zahanati ili kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda katika hospitali teule ya Makandana ambako wamekuwa wakilazimika kutumia gharama kubwa za usafiri hususani nyakati za usiku wanapopeleka wagonjwa.
Kutokana na hali hiyo,mkuu wa mkoa amesema hayuko tayari kuona tofauti za kisiasa baina ya uongozi wa kata na kijiji zikiendelea kukwamisha maendeleo ya wananchi hivyo pande hizo zinapaswa kushirikiana na uongozi wa wilaya kutatua changamoto iliyopo.