Jumamosi , 22nd Mei , 2021

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Elimu na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanayatunza magari waliyokabidhiwa na serikali na kwamba atakayekutwa amepaki gari kisa kukosa 'service' atakuwa hana kazi na kwamba magari hayo yasitumike kununulia nyanya wala kwenda nayo bar.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Kauli hiyo ameitoa jana Mei 21, 2021, wakati akikabidhi jumla ya magari 184 yenye thamani ya shilingi bilioni 16.4, kwa maafisa elimu wa Halmashauri ikiwa ni mkakati wa serikali ya awamu ya sita kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini na kuzitaka Halmashauri zilizopokea magari hayo kuzingatia taratibu za serikali katika matumizi na matengenezo ya magari hayo.

"Magari haya mmekabidhiwa, maafisa elimu na wakurugenzi wa Halmashauri, tukute gari limepaki kisa limekosa ‘Service’ utakuwa umekosa kazi, lazima tuambizane ukweli, magari haya lazima yafanye kazi kwa zaidi ya miaka mitano hadi sita, na yatumike kwa ajili kufuatilia masuala ya elimu, haya siyo magari ya kwenda kununulia nyanya, wala kupumzika nayo Bar", alisema Waziri Mkuu

 Amesema kuwa magari hayo ni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ufuatiliaji na tathmini kwa Maafisa Elimu, na yametolewa na serikali ili yasaidie kuharakisha shughuli za utekelezaji wa majukumu katika sekta ya elimu.