Jumatatu , 8th Feb , 2016

Wizara ya fedha na Mipango, leo imetimiza ahadi ya Rais John Pombe Joseph Magufuli, aliyoitoa katika kilele cha siku ya mahakama nchini juma lililopita; ya kuipatia idara ya mahakama kiasi cha shilingi bilioni 12.3 kwa ajili shughuli za maendeleo.

Waziri wa fedha na uchumi Dkt Philip Mpango

Waziri wa fedha na uchumi Dkt Philip Mpango, amemkabidhi naibu katibu mkuu wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju, hundi ya kiasi hicho cha fedha kama ishara ya kutimia kwa ahadi ya Rais Magufuli, katika hafla iliyofanyika makao makuu ya wizara ya fedha jijini Dar es salaam.

Akizungumza mara baada ya kupokea cheki hiyo, Naibu Katibu Mkuu Mpanju amesema watahakikisha wanazitumia fedha hizo kwa ajili ya shughuli iliyopangiwa ikiwa ni pamoja na kuharakisha usikizwaji wa kesi zinazohusu masuala ya biashara na kodi.

Kwa upande wake, mtendaji mkuu wa mahakama Bw. Hussein Katanga ametaja miradi mingine ya maendeleo itakayotekelezwa kupitia fedha hizo kuwa ni ujenzi wa majengo mapya ya mahakama kabla ya kuisha kwa mwaka wa bajeti wa serikali.