
Mahakama Kuu nchini Kenya imekataa ombi lililowasilishwa na Michael Onyango Otieno, la kusitisha agizo la kuzikwa kwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga, ndani ya saa 72, kwa madai kuwa kuharakishwa kwa mazishi ya Odinga kunakiuka Katiba ya Kenya, hasa Kifungu cha 44, kinachohakikisha haki ya kila mtu kushiriki katika maisha ya kitamaduni ya jumuiya yao.
Akitoa uamuzi huo jana, Alhamisi, Oktoba 16, 2025, Jaji Chacha Mwita amesema kuwa mleta maombi hakuonyesha uhitaji wa dharura wa kuingilia kati mchakato wa mazishi hayo na hakuweza pia kuthibitisha kama maandalizi ya mazishi yalikuwa yakifanywa kinyume na matakwa ya marehemu.
Awali, Otieno aliitaka mahakama itamke kuwa utaratibu huo wa maziko unakiuka haki za wananchi wanaotaka kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa upinzani aliyekuwa na mchango mkubwa katika siasa za nchi hiyo akiwa na ushawishi mkubwa hususani kwa vijana.