Ijumaa , 21st Nov , 2014

Bunge limesema hakuna barua ya mahakama iliyolizuia kujadili jambo lolote likiwemo sakata la wizi wa fedha za Tegeta Escrow.

Mwenyekiti wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu

Siku moja baada ya wabunge kupinga hatua ya kutaka kutumia Mhimili wa mahakama kuzuia mjadala wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow bungeni, bunge limesema hakuna barua ya mahakama iliyolizuia kujadili jambo lolote likiwemo sakata la wizi wa fedha za Tegeta Escrow.

Akitoa maelezo hayo bungeni, mwenyekiti wa kikao cha 14 cha bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu amewataka wabunge kuacha kuzungumzia swala la barua hiyo kwa kuwa hakuna barua yoyote ya mahakama iliyozuia na mahusiano kati ya mihimili hiyo miwili itaendelea kuwa mazuri.

Hatua hiyo ya mwenyekiti wa kikao hicho imekuja kufutia msemaji wa kambi ya upinzani Mhe. Moses Machali kusema njama za kuzuia sakata la Escrow kujadiliwa bungeni linalenga kuwalinda viongozi wa serikali na taasisi zake waliohusika na wizi huo jambo ambalo ni hatari kwa mustakali wa taifa.

Wakichangia azimio la bunge la kuridhia itifaki ya uzuiaji wa vitendo haramu dhidi ya miundombinu ya kudumu iliyojengwa chini ya bahari katika mwambao wa bara la Afrika 1988, baadhi ya wabunge wamedai kuharakishwa kuridhiwa kwa azimio hilo baada ya kutoletwa katika bunge kwa zaidi ya miaka 26 ni kutokana na zoezi la utafutaji mafuta na gesi jambo ambalo serikali ilitakiwa kuacha wazi.

Akifafanua hoja za baadhi ya wabunge baada ya kuwasilisha azimio hilo,waziri wa uchukuzi Mhe. Dkt Harrison Mwakyembe amesema nchi 140 zimeridhia azimio la kuridhia itifaki hiyo ambayo inalenga nchi wanachama wa itifaki kuwa na mikakati ya pamoja ya kulinda usalama wa miundombinu na maisha ya watu walioko kwenye miundombinu pamoja na kuweka adhabu kulinda uhalifu.