Jumanne , 25th Jun , 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, amesema Taifa Stars, inahitaji kupewa licha ya kupoteza kwa bao 2-0 dhidi ya Senegal, kwenye mchezo wake wa kwanza kwenye michuano ya AFCON inayoendelea nchini Misri.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo,  jijini Dar es salaam, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa ghala la taifa la mitambo ya gesi nchini, ambapo ameeleza wachezaji hao wa Taifa stars walijitahidi katika mchezo huo.

"Kwenye uwanja wa mpira kuna kushinda na kushindwa kwahiyo wao wakazane, wajitume zaidi na sisi tuendelee kuwaombea, mimi nina uhakika hata huo mwanzo sio mbaya sana, kufungwa magoli mawili tu na timu ambayo inaongoza Afrika sio jambo baya, tuendelee kuwapa moyo" amesema Rais Magufuli.

Awali Mkuu Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameeleza, kuumizwa na tabia ya baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii kuoneshwa kuwabeza wachezaji wa timu ya taifa.

"Nilikuwa natamani kuomba kibali angalau niende tu kule kambini lakini ikikupendeza Mh. Rais utajua mwenyewe utakavyoamua. Najisikia faraja vyombo vyote kule vinatangaza habari ya Tanzania, leo tunasema hawana lolote, hawana lishe, maneno haya ya kukatisha tamaa hayana tija" amesema Paul Makonda.