Jumatatu , 18th Dec , 2017

Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. John Pombe Magufuli amesema hana mpango wa kubadilisha Sekretarieti ya chama hicho na itaendelea kama ilivyo chini ya Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana.

Mwenyekiti huyo mpya amechaguliwa kwenye mkutano wa tisa wa chama hicho uliomalizika jioni hii mjini Dodoma kwa kupata kura zote 1821 za wajumbe wa mkutano mkuu. Rais Magufuli atahudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitano kuanzia leo hadi mwaka 2022 utakapofanyika uchaguzi mwingine.

Katika hotuba yake baada ya kuchaguliwa Dkt. Magufuli amesema kwasasa hana mpango wa kubadilisha Sekretarieti na itaendelea kama ilivyo chini ya katibu mkuu wa Chama hicho Ndugu Abdulrahman Kinana.

Matokeo ya Uchaguzi huo yametangazwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai ambaye amewataja washindi wote katika nafasi za Mwenyekiti Taifa, Mwenyekiti Zanzibar na Makamu Mwenyekiti Taifa. 

Mbali na Mwenyekiti wa Taifa lakini pia Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ameshinda nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa kura zote 1821 wakati Ndugu Philip Mangula akishinda nafasi ya Makamu mwenyekiti Taifa kwa kura zote 1821.