Alhamisi , 22nd Oct , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dkt. John Magufuli, amesema kuwa ameona takwimu za dunia nzima kuhusu maambukizi ya virusi vya Corona zilizotolewa na gazeti la New York Times la nchini Marekani, ambapo limeonesha kuwa Tanzania haina kabisa maambukizi ya ugonjwa huo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.

Magufuli, amesema hayo hii leo, Oktoba 22, 2020, alipokuwa akifanya ufunguzi wa kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro, wakati akisisitiza suala la amani, na kwani amani isingekuwepo na hata wawekezaji katika kiwanda hicho wasingefika.

"Hata vurugu ya Corona ambayo nayo ilikuwa inatupunguzia amani Mungu aliiokoa, nilikuwa naangalia 'information' za gazeti moja la Marekani la New York Time, wametoa ramani ya dunia nzima, nchi pekee ambayo haina corona ni Tanzania, yaani picha yake ni nyeupe pee, zingine zote zina rangi tunachotakiwa tuitunze amani, mapya mengi yanakuja", amesema Magufuli.

Aidha Rais Magufuli akatoa rai kwa Mawaziri na Watanzania kiujumla kuhakikisha wananunua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini, "Nitashangaa sana kama vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vitanendelea kuagiza viatu kutoka nje, nitashangaa sana mawaziri, wakiongozwa na mimi Rais, Waziri Mkuu na Makatibu Wakuu tusipovaa viatu vinavyotengenezwa hapa Karanga".