Jumapili , 29th Jan , 2017

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli, leo ameweka historia mpya katika makao makuu wa Umoja wa Mataifa ya Afrika (AU) kwa kuongoza ufunguzi rasmi wa jengo la kituo cha amani lililopewa jina la Mwalimu Julius Nyerere na kuhutubia kwa lugha ya Kiswahili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akiwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta pamoja na viongozi wa mataifa mabalimbali wakiwa katika picha ya pamoja katika jengo jipya la kituo cha Amani na Usalama (JULIUS NYERERE) lililopo katika Makao makuu ya Umoja wa Afrika Addis Ababa nchini Ethiopia.

Jengo hilo la amani na usalama lililopo makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia leo tarehe 29 Januari, 2017 limetangazwa rasmi kuwa litaitwa Mwalimu Julius Nyerere.

Jengo hilo limepewa jina hilo rasmi katika hafla ya chakula cha mchana iliyofanyika leo na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Marais mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Antonio Guterres, Mawaziri na Mabalozi mbalimbali wanaohudhuria Mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaoendelea Mjini hapa.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote wa Umoja wa Afrika kwa kuamua jengo hilo liitwe jina la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni kutambua mchango wake katika kupigania amani na usalama na amebainisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwahutubia Viongozi Wakuu wa Mataifa mbalimbali hawapo (pichani) katika Jengo jipya la Kituo cha Amani na Usalama kilichopewa jina Rasmi la Mwalimu Julius Nyerere, Addis Ababa nchini Ethiopia

“Na kwa hakika naweza kusema kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora kabisa ambaye amewahi kutokea katika Bara letu, katika maisha yake yote Mwalimu Nyerere alipambana ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Afrika, alikuwa mmoja wa waanzilishi wa umoja huu, sisi Watanzania kwa hakika tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Dkt. Magufuli ameongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika kupambana na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika, na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa Taifa la Tanzania aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika nchi za Afrika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akijadiliana jambo na Rais wa Rwanda Paul Kagame wakati wakielekea katika Kituo cha Amani na Usalama cha Makao Makuu ya Umoja wa Afrika kilichopewa jina la Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere, Addis Abba nchini Ethiopia. 

“Wito wangu kwenu, waheshimiwa viongozi ni kwamba, sambamba na kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama tutajitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya viongozi wengine hodari wa Bara hili wakiwemo Hayati Kwame Nkhrumah, Ahmed Ben Bella, Sekou Toure, Gamal Abdel Nasser na bila kusahau shujaa wetu mwingine Hayati Nelson Mandela” amesisitiza Rais Magufuli.

Mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaendelea kesho tarehe 30 Januari, 2017 hapa Addis Ababa.