
Dereva na abiria
Kufuatia suala hilo, uongozi wa Umoja wa Waendesha Bodaboda mkoani Njombe umewataka madereva wanaosafirisha abiria kuhakikisha wanachukua hatua stahiki kwa abiria wanaokataa kuvaa kofia hizo ili kulinda usalama wao.
Imeelezwa kuwa baadhi ya abiria mjini Njombe wamekuwa hawapendi kuvaa kofia ngumu wakati wakisafiri na bodaboda kwa madai kuwa madereva wa vyombo hivyo hawazingatii usafi wa kofia, suala ambalo Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda mkoani humo, Philimon Mwinuka amelitolea maelezo.
"Akifika abiria mkaribishe vizuri, akikataa kofia ngumu we usibishe, mbebe nenda naye barabarani lakini madereva wenzako wawe wanajua ili hata kama ukikamatwa basi utaeleza ukweli na wenzako watakuwa mashahidi, ili mzigo uwe kwake", amesema Philimon.
Baadhi ya madereva wa Bodaboda mjini Njombe walioshiriki mkutano ulioitishwa na uongozi wa waendesha bodaboda, wametoa kilio kwa wauzaji wa pikipiki kuhakikisha kofia zinazopendekezwa zinapatikana kwa wingi. Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Njombe, Jane Warioba akiongoza mafunzo ya matumizi ya namna ya kuvuka vivuko vya watembea kwa miguu, amesema kila dereva anayeendesha chombo cha moto wakiwemo anapaswa kutii matumizi ya alama za barabarani ikiwemo kuzingatia uvaaji wa kofia ngumu.