
Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa.
Wakizungumza katika mkutano wa kampeni hizo, zilizofanyika uwanja wa soko la Monduli, viongozi wengi wa CCM walisisitiza kuwa Lowassa ndiye aliyekuwa sababu ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema kuondoka na kurejea tena CCM.
Kwa upande wake aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli na Diwani wa Monduli mjini, Isack Joseph ambaye hivi karibuni alijiuzulu udiwani na kujiunga CCM, amesema kabla ya uamuzi huo alikwenda mara tatu kuonana na Lowassa.
Wakati huo huo Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wakati akizindua kampeni za jimbo la Monduli, katika Kata ya Mto wa Mbu, kumnadi mgombea wa chama chake Yonas Laiser amewataka wananchi kupuuza propaganda kuwa Chadema itakufa na yeye kuhamia CCM.
Lowassa huku akielezea maendeleo aliyoleta Monduli katika kipindi chake cha ubunge cha miaka 20, amesema aliingia ubunge wa Monduli kukiwa na shida ya maji, barabara, umeme na ardhi lakini alishughulikia na leo kila Mtanzania anajua.
"Chadema bado tupo imara na tutashinda kitendo cha kujiuzulu aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga kilikuwa cha hovyo na kimeniudhi na kunikasirisha sana”, amesema Lowassa.
Edward Lowassa ni waziri mkuu wa zamani ambaye alihamia Chadema mwaka 2015, mara baada ya kukatwa jina lake katika kikao cha kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) alipokuwa akiwania nafasi ya kugombea Urais.