Alhamisi , 22nd Aug , 2019

Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina Abdulrazak Hamis (2), mkazi wa Kijiji cha Njinjo wilayani Kilwa, ameungua kwa moto sehemu kubwa mwilini mwake, kufuatia kuachwa karibu na moto na mama yake Mzazi.

Akizungumzia hali ya mtoto huyo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Lindi Dr. Albert Chotta, amesema hali yake si nzuri kutokana na kuungua asilimia 90 ya mwili wake, huku akitoa wito kwa wazazi kuwa makini na majanga ya moto.

Katika mahojiano maalum na EATV & EA Radio Digital, Daktari huyo amesema Abdullazaki Hamisi, amelazwa wodi namba 1 katika Hospitali ya Mkoa wa Lindi, akipatiwa huduma za tiba kutoka kwa wataalamu, huku ikielezwa karibu robo tatu ya mwili wake ukiwa umeungua moto huo.

Kwa upande wake Mama mzazi wa mtoto huyo, Salma Hamisi, amesema baada ya kumaliza kumuogesha mtoto huyo aliamuacha karibu na moto ili apate joto ndipo moto ukashika nguo alizokuwa amevaa na kuanza kuungua, huku yeye akiwa nje ya nyumba bila kujua kinachoendelea ndani.