Alhamisi , 15th Jan , 2015

Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu wa ngozi (TAS) mkoani Dodoma, Ludovick Kowo amesema kitendo cha serikali kupiga marufuku waganga wa kienyeji wanaopiga ramli ili kuepusha mauaji ya albino nchini ni fedheha kwa jamii hiyo.

Baadhi ya Viongozi wa Chama cha watu Wenye Ulemavu wa Ngozi Tanzania(TAS)

Kowo alitoa kauli hiyo leo mjini hapa wakati akizungumza na East Africa Radio kuhusiana na kauli ya serikali ya kuwapiga marufuku wapiga ramli nchini ili kuepusha mauji ya albino kwani imebainika kuwa wao ndiyo chanzo cha mauaji hayo.

Amesema serikali inayajuwa makundi ya watu ambayo yamekuwa yakitumia viungo vya albino kwa ajili ya kujitajirisha na kupata mafanikio ya haraka hivyo kuwapiga marufuku wapiga ramli nchini ni danganya toto kwa albino.

“Ni nani asiyejua kuwa wanasiasa na wafanyabiashara nchini ndiyo wanaoongoza kwa mauaji ya albino na serikali inalijua hilo lakini haitaki kuchukua hatua madhubuti ya kuwalinda na badala yake sasa imekuja na mkakati wa kuwapiga marufuku wapiga ramli… kwa maoni yangu mimi marufuku hii haitasaidia hata kidogo kuzuia mauaji ya albino,” amesema Kowo.

Ameongeza kuwa, “Kama kweli serikali inataka kukomesha mauaji ya albino nchini ni lazima ipige marufuku watu wote wanaojishughulisha na shughuli za uganga wa kienyeji kwani huko huko ndipo kulipo na wapiga ramli lakini bila hivyo albino wataendelea kuuawa kila siku.”

Aidha amesema katika matukio ya hatari yanayotokea hapa nchini na duniani kwa ujumla serikali huamua kutenga mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwalinda wananchi wake lakini linapokuja suala la mauaji ya albino serikali haijatenga hata shilingi kumi kwa ajili ya kuwalinda.

“Mfano mzuri tu ni pale ulipozuka ugonjwa wa ebola serikali ilitenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo lakini linapokuja suala la kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi inaleta mzaha utafikiri siyo raia wake,” alisema Kowo.

Amesema kitendo cha serikali kupiga marufuku wapiga ramli siyo mzizi wa kumaliza mauaji ya albino kwani ramli ni siri ya mganga na aliyekwenda kutibiwa hivyo ili marufuku hiyo ifanikiwe ni lazima serikali iwe makini sana katika kukabiliana na watu hao.

Kwa upande wake katibu wa Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu (Shivyawata) mkoa wa Dodoma, Justus Ng’wantalima amesema hiyo ni hatua nzuri kwa serikali kukabiliana na mauaji ya albino ambayo yamechafua sifa ya nchi kimataifa.

Na kuitaka serikali kufuatilia kwa ukaribu marufuku hiyo ili iweze kufanikiwa kwa kuwa kuna baadhi ya watu ambao wamejiajiri katika kazi hiyo hivyo kuwapiga marufuku haitakuwa rahisi kuiacha kazi hiyo.