
Wananchi wakiwa kwenye banda la NIDA wakijiandikisha kwaajili ya kupata vitambulisho.
Akizungumza na www.eatv.tv Mkuu wa kitengo cha mawasiliano NIDA, Rose Mdami, amesema kuwa mamlaka imeelekeza vitambulisho vyote vitumike na endapo zoezi la kubadili vitambulisho litafanyika, itakuwa baadaye baada ya kukamilisha usajili nchi nzima.
“Zoezi la kubadili vitambulisho vya awali kama litafanyika ni baadaye sana, kwani zoezi hilo litagharimu fedha kwa mantiki hiyo tunapunguza gharama kwa serikali na tumeunda kitu kinachoitwa tovuti salama ambayo itakayomsaidia mtu kutumia kitambulisho cha awali na taarifa zake zikaonekana na tovuti hii inaweza kutumiwa na mamlaka zote zitakazo hitaji taarifa za mhusika”, amesema Mdami.
Hayo yanajiri ikiwa ni miaka miwili tangu kutoka kwa tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazaniana Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuitaka Mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) kuhakikisha inabadilisha vitambulisho kwa kila mwananchi kutokana na vitambulisho vya awali kukosa sahihi ya mmiliki.