Jumapili , 2nd Mar , 2025

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake, hakuna mfano bora wa mwanamke shupavu, mwenye maono na anayevunja vikwazo kuliko Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Safari yake ya uongozi si tu fahari kwa Tanzania bali pia ni mwangaza kwa wanawake duniani wanaotamani kushika nafasi za juu za maamuzi.  

Uongozi wa kiutendaji na maono thabiti 
Tangu aingie madarakani mwaka 2021, Rais Samia ameonesha kuwa wanawake wanaweza kuongoza kwa weledi, hekima, na maono makubwa. Kupitia sera zake za mageuzi, Tanzania imeendelea kukua kiuchumi, kidiplomasia na kijamii.  

Katika sekta ya uchumi, Rais Samia ameendeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), bwawa la umeme la Julius Nyerere, na upanuzi wa bandari na viwanja vya ndege. 

Mwanamke bingwa wa diplomasia  
Katika medani za kimataifa, Rais Samia ameiboresha sura ya Tanzania kwa ulimwengu. Ameshuhudia Tanzania ikipokea wawekezaji wakubwa, misaada ya maendeleo, na kushirikiana na mataifa makubwa kwa maslahi ya nchi. Kupitia falsafa yake ya 4Rs – Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya, amerejesha mshikamano wa kitaifa na kuimarisha demokrasia bila kuyumbisha msingi wa uthabiti wa nchi.  

Mhamasishaji wa Wanawake na Vijana  
Rais Samia amekuwa kinara wa kuwawezesha wanawake kwa vitendo. Katika uongozi wake, tumeshuhudia ongezeko kubwa la wanawake walioteuliwa kushika nyadhifa za juu serikalini, mashirika ya umma na sekta binafsi. Amewahamasisha wanawake wa Tanzania na Afrika kuthubutu kuwania nafasi za juu bila hofu wala kujiona duni.  

Kupitia miradi kama "Jasiri Fund" na program za uwezeshaji wa wanawake wajasiriamali, amehakikisha wanawake wanapata mtaji na fursa za kuinua maisha yao kiuchumi. Hili linaakisi dhamira yake ya kweli ya kutetea haki za wanawake sio kwa maneno bali kwa vitendo.  
 
Katika siku hii adhimu ya kimataifa ya wanawake, tunajivunia kuwa na Rais Samia Suluhu Hassan kama mfano wa kuigwa, yeye ni ushahidi hai kwamba mwanamke anaweza, mwanamke anastahili, na mwanamke ana uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii yake na dunia kwa ujumla.  

Tanzania ina bahati kuwa na kiongozi jasiri kama yeye na kwa kila binti anayetamani kuwa kiongozi, kwa kila mama anayepigania kesho bora, na kwa kila msichana mwenye ndoto kubwa, Rais Samia ni ishara kwamba hakuna lisilowezekana!