Jumapili , 7th Feb , 2016

Licha ya katazo kubwa kutoka kwa Umoja wa Mataifa na nchi pinzani ya Korea Kusini, Korea Kaskazini imerusha kombora la masafa marefu angani, na kusababisha shutuma za kimataifa.

Vyombo vya habari vya Korea Kusini vimesema kuwa kombora hilo lilipitia anga ya Japan katika kisiwa cha Okinawa.

Rais wa Korea Kusini Park Geun-hye amesema kuwa kitendo hicho ni cha uchokozi na kutaka hatua kali kuchukuliwa dhidi ya Korea Kaskazini.

Naye waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa marekani John Kerry amesema kuwa uzinduzi huo hauhatarishi tu usalama wa rasi ya Korea, bali eneo lote pamoja na Marekani.

Pia waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe ametaja jaribio hilo ni kitendo ambacho hakiwezi kuvumiliwa, na kwamba ni ukiukaji wa azimio la umoja wa mataifa.

Licha ya Korea Kaskazini kusema kuwa nia yake ilikuwa ni kupeleka chombo hicho katika sayari ya mbali, wakosoaji wake wanaamini kuwa Korea inatengeneza zana za kinyuklia zenye uwezo wa kufika nchini Marekani.