Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa anafurahishwa na kiwango cha uwekezaji wa makampuni ya Jamhuri ya Watu wa China katika uchumi wa Tanzania ambao hadi mwishoni mwa mwaka jana ulikuwa umefikia miradi 522 yenye thamani ya dola za Marekani 2,490.21 milioni (dola bilioni 2.5).
Rais Kikwete amesema kuwa kiwango hicho kinaufanya uwekezaji wa China katika Tanzania kushika nafasi ya tano, kwa thamani ya fedha, na kuwa uwekezaji huo utaiwezesha Tanzania kupata ajira 77,335 baada ya kukamilika kwa miradi yote kukamilika ambayo ujenzi wake unaendelea.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa uzuri wa uwekezaji huo kutoka China ni kwamba miradi mingi, 354 kati ya miradi hiyo yote 522 ya wafanyabiashara kutoka China ni kwenye sekta ya uzalishaji.
Rais Kikwete amesema hayo leo, Alhamisi, Oktoba 23, 2014, wakati alipofungua Mkutano wa Tatu wa Uwekezaji wa Tanzania na China (Third Tanzania-China Investment Forum) kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Nyumba ya Kulala Wageni ya Serikali ya Diaoyutai mjini Beijing, China ambako Rais anafanya ziara ya Kiserikali.
Akizungumza na mamia kwa mamia ya wafanyabiashara ambao walijaa kwenye ukumbi huo, Rais Kikwete amesema kuwa uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na China umekua mno kiasi cha kwamba kati ya Julai na Septemba mwaka huu, 2014, thamani ya miradi imefikia dola za Marekani milioni 533.9 kulinganisha na miradi yenye thamani ya dola za Marekani 124.14 kwa kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka jana.
Rais Kikwete amesema kuwa ongezeko hilo lilifuatia kufanyika kwa Mkutano wa Pili wa Uwekezaji Kati ya Tanzania na China uliofanyika Dar Es Salaam Juni 23 hadi 25, mwaka huu, wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa China katika Tanzania, Mheshimiwa Li Yuanchao ambaye aliambatana na wafanyabiashara 100.
Rais Kikwete amesema pia kuwa biashara kati ya Tanzania na China imeongezeka lakini kwa kutilia maanani ukubwa wa uchumi wa China ambao ni wa pili duniani kwa ukubwa, bado biashara hiyo inaweza kukua zaidi.
“Kwa mwaka 2012/2013, kwa mfano, biashara kati ya nchi hizo ilikuwa na thamani ya dola za Marekani 1,595.16. Kati ya hizo, mauzo ya bidhaa za China kwa Tanzania zilikuwa sawa na dola 1,099.42 wakati China ilinunua kutoka Tanzania bidhaa zenye thamani ya dola milioni 495.74. Lakini ni dhahiri kuwa tunaweza kufanya vizuri,” alisema Rais Kikwete.