Alhamisi , 29th Oct , 2015

Mkuu wa wilaya ya Arusha mjini, Fadhili Nkurlu, amepiga marufuku uuzwaji wa vyakula katika mazingira machafu, matunda na vimiminika vingine kwa muda usiojulikana, kutokana na ugonjwa wa kipindupindu kuingia wilayani humo.

Mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini, Fadhili Nkurlu

Nkurlu amesema ugonjwa huo umeanza Wiyani hapa, Oktoba 5 mwaka huu, ambapo mwananchi mmoja kutoka Mkoani Singida, kuanza kuharisha na kutapika akiwa safarini kuja Jijini Arusha na alipopelekwa hospitalini vipimo vilithibitika kuwa alikuwa na ugonjwa huo.

Aidha amesema kwa sasa wodini kuna wagonjwa watano kwenye kituo cha afya cha Levolosi na wagonjwa watatu, kati yao wanatoka mkoani Singida, mmoja ni kutoka malmashauri ya wilaya ya Arusha, mmoja kutoka halmashauri ya Simanjiro, huku wagonjwa wengine 22 wakitokea halmashauri ya jiji la Arusha.

Amesema hata hivyo mgonjwa huyo alitibiwa na kuruhusiwa nyumbani, lakini kuanzia wakati huo hadi sasa idadi ya wagonjwa wa ugonjwa huo imeongezeka na kufikia 27.

Naye mkurugenzi wa jiji la Arusha, Juma Idd amesema, hadi sasa kata nne ambazo ni za Sinon, Darajani, Kimandolu na Sombetini ndizo zimeathirika na ugonjwa huo.

Pia ugonjwa huo unadhibitiwa kwa kuchemsha maji safi na salama, pamoja na kutumia sawa aina ya chlorine (water guard), kunawa mikono baada ya kutoka chooni na kabla ya kula, kujenga choo umbali wa mita 30 kutoka chanzo cha maji.