Ijumaa , 4th Aug , 2023

Kiongozi wa Niger aliyeondolewa madarakani ameitaka Marekani na jumuiya ya kimataifa kusaidia kurejesha katiba ya nchi hiyo.

 

Katika makala ya maoni kwenye gazeti la Washington Post, Rais Mohamed Bazoum alisema alikuwa akiandika "kama mateka".  Pia alionya kwamba nchi hiyo inaweza kuanguka zaidi chini ya ushawishi wa Urusi, kupitia kundi la Wagner ambalo tayari linafanya kazi katika nchi jirani.

Majirani wa Niger katika eneo la Afrika Magharibi wametishia kuingilia kati kijeshi.Siku ya Alhamisi, viongozi wa mapinduzi walitangaza kuwa wanawaondoa mabalozi wa nchi hiyo kutoka Ufaransa, Marekani, Nigeria na Togo.

Katika taarifa iliyosomwa kwenye televisheni ya taifa, walisema kuwa kazi za mabalozi hao wanne zimesitishwa. Saa chache kabla, balozi wa Niger nchini Marekani, Kiari Liman-Tinguiri, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba serikali ya nchi hiyo inapaswa kuwa na mantiki na kutambua kwamba suala hili haliwezi kufanikiwa.

Niger ni mzalishaji mkubwa wa madini ya urani  mafuta ambayo ni muhimu kwa nguvu za nyuklia na chini ya Bwana Bazoum alikuwa mshirika muhimu wa nchi za Magharibi katika vita dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi.

Katika makala yake ya gazeti, Bw Bazoum alionya mapinduzi hayo, iwapo yatafanikiwa, yatakuwa na athari mbaya kwa nchi hiyo na dunia nzima.