Jumanne , 25th Jul , 2023

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana amezulu kaburi la hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na kusema kuwa ni mwanamapinduzi wa kweli na shujaa wa Afrika.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akiweka shada la maua kwenye kaburi la Hayati Baba wa Taifa

Amesema wakati Tanzania ikiadhimisha siku ya mashujaa, Mwalimu Nyerere anabaki kuwa shujaa namba moja wa Tanzania huku pia akimtembelea Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mstaafu Jenerali David Musuguli (103) na kumwelelezea kuwa ni alama ya uzalendo wa Taifa, ni alama ya ukombozi na anastahili kuombewa afya njema.

Kanali Mstaafu Kinana ameyasema hayo leo Julai 25, 2023 baada ya kuzulu kaburi la Mwalimu Nyerere na kumtembelea Mzee Musuguli nyumbani kwake Butiama mkoani Mara akiwa katika ziara kukagua uhai wa Chama,  utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuzungumza na wanachama.

Akiwa nyumbani kwa Jenerali Musuguri, Kinana alimwelezea kuwa mzalendo wa kweli aliyeongoza mapambano dhidi ya Idd Amin.

"Jenerali Musuguli ameliongoza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa zaidi ya miaka 50, ameliongoza Jeshi katika nafasi mbalimbali, wakati leo tunaadhimisha miaka 44 ya vita ya Uganda Jenerali Musuguli ndiye aliyeyaongoza majeshi ya Tanzania kumng'oa Nduli Idd Amin," amesema.