Jumanne , 26th Aug , 2014

Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania kesho anatarajiwa kufungua mkutano wa kwanza na kikao cha tatu cha Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki kitakachofanyika jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Karimjee.

Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Dkt. Margaret Nantongo Zziwa amesema mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano huo wabunge watajadili miswada kadhaa ambayo ipo mbele ya kamati za bunge hilo ikiwa ni pamoja na muswada wa elimu.

Kwa upande wao Mbunge wa bunge hilo kutoka nchini Rwanda Mh. Patricia Hajabakiga na Mbunge wa Tanzania katika bunge la Afrika Mashariki Mh. Adam Kimbisa wamezungumzia umuhimu wa kikao hicho kufanyika jijini Dar es Salaam na si katika jiji la Arusha ambapo ndiko Makao Makuu ya Jumuiya hiyo.

Kwa Mujibu wa Kimbisa, hatua hiyo ni mwanzo wa utekelezaji wa maadhimio yaliyofikiwa hivi karibuni ambapo ilikubaliwa kuwa kila nchi mwanachama ipate fursa ya kuwa mwenyeji wa vikao vya bunge hilo, vikao vitakavyofanyika kwa utaratibu wa mzunguko.