Jumanne , 16th Jul , 2024

Kijana aliyefahamika wa jina la Lisborn Adam Selemani ­(16) mkazi wa mtaa wa Nyerere Road Kata ya Kalangalala Halmashauri ya mji Geita mkoani Geita ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na vijana wanaosadikika kuwa ni marafiki zake.

Akizungumza na EATV Baba mzazi wa kijana huyo Adam Selemani amesema kijana wake alichomwa na kitu kinachosadikika kuwa ni kisu wakati akiwa na marafiki zake majira ya jioni siku ya jumapili ya julai 7 2024 wakiwa maeneo ya machinjio ya zamani mtaa wa ujamaa kijana huyo alivyopelekwa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Geita iliyopo magogo alifanyiwa upasuaji mara tatu ndipo siku ya jumapili ya julai 14 kijana huyo alipoteza maisha.

“Kijana wagu alivyonisimulia wakati yupo hospitali alisema alivyochomwa baada ya kumpata tukio hili alitaka akimbie akajua amejeruhiwa kidogo lakini alishindwa akaanguka barabarani kuna mama mmoja ndo alimkuta akiwa analilia maumivu akamwambia bodaboda mpeleke mtoto huyu hospitali inaonekana kajeruhiwa walifikiri kachomwa na chuma kumbe ni kisu alifanyiwa oparasheni baadae ikagundulika anachangamoto kwenye utumbo maana kinyesi alikuwa anatolea mdomoni na sehemu ya haja kubwa”ADAM SELEMAN-Baba wa Marehemu

“Tulikaa hospitali siku ya kwanza siku ya pili hali ikazidi kuwa mbaya zaidi ikabidi afanyiwe oparesheni tena ya mara ya tatu nipo alipotolewa ile juzi jana kashida vizuri ili ilipofika saa tatu usiku hali ikabadilika ndo hivyo tukampoteza”SAPINAA DANIEL-Shangazi wa Marehemu

Majirani wa familia hiyo wanaelezea jinsi walivyopokea taarifa ya tukio hilo.

“Mimi taarifa za tukio hili nilizipata majira ya saa sita usiku hivi nikapigiwa simu na jirani yangu ananiambia Yule kijana wa Adam aliyechomwa kisu amefariki tukabaki kwenye mshangao tu yaani inauma sana”SHAMIMU ABDALLAH-Mkazi wa Mtaa wa Nyerere road

“Jumamosi tulienda kumwona hospitali hali ikawa inaridhisha ilipofika jana hali ikabadilika na usiku siku ya jumapili akawa amepoteza maisha”MWAJABU OMARY-Mkazi wa Mtaa wa Nyerere Road

“Tunaliomba sana jeshi la polisi lifatilie hivi vikundi ambavyo vipo kwenye maeneo yetu na havina kazi maalumu watu wako humu wanajiita mbwa mwitu wanajiita wasela hao hao ndo wanasababisha mauti kama haya”PATRICK PAULO-Polisi jamii mtaa wa Nyerere Road

Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Nyerere Road George Maguga amesema mpaka sasa uongozi wa mtaa huo kwa kushirikiana na Polisi kata kata ya kalangalala waliwakamata vijana watatu kwa tuhuma za tukio hilo.

“Baba wa familia akiwa hospitalini na Kijana wake alimtajia baadhi ya majina ya vijana wenzake alikuwa nao wakati tukio linatokea alitutajia hayo majina na sisi tukafanya kazi ya kufatilia hayo majina bahati nzuri tukafanikiwa kuwakamata vijana watatu ambao nilimshirikisha afisa mtendaji wa kata na Polisi Kata tukawachukua na kuwapeleka kituo cha polisi”GEORGE MAGUGA-Afisa Mtendaji wa mtaa wa Nyerere Road

Jeshi la polisi lilifika nyumbani kwa marehemu na kuzungumza na baba wa familia ikiwa ni sehemu ya kuendelea na uchunguzi wa tukio hilo.