
Abdul Nsembo (Fulana nyeupe) na Shamim Mwasha (wa mbele kushoto).
Kesi ya usafirishaji wa madawa ya kulevya inayomkabili, Shamim Mwasha (41) na Mumewe Abdul Nsembo maarufu kama Abdulkandida (45) imetajwa leo June 24, katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu na kuelezwa kuwa kinachosubiriwa ni ripoti ya kielelezo kutoka kwa mkemia mkuu wa serikali.
Wakili wa serikali Wankyo Saimon, amesema hayo mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi Kelvin Mhina, Kesi hiyo namba 36 ya mwaka 2019, imeshindwa kuendelea mahakamani hapo baada ya upande wa mashtaka kudai kwamba unasubiri ripoti ya mkemia mkuu ambapo washtakiwa hao wanashitakiwa kwa kosa moja la usafirishaji wa madawa ya kulevya aina ya Heroin.
Wakili Wankyo, amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba kesi hiyo kuahirishwa ambapo upande wa utetezi umeomba kupewa taarifa ya lini ripoti hiyo itakamilika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 8 mwaka huu, ambapo washtakiwa wamerudishwa rumande.
Shamim na mumewe wanatajwa kutenda kosa hilo Mei Mosi mwaka huu, wakiwa nyumbani kwao maeneo ya Mbezi beach, ambapo walikutwa na dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa gramu 232.70 kinyume na sheria ya uhujumu uchumi.