Alhamisi , 9th Apr , 2015

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja leo amefikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali ya kesi inayomkabili ya uchochezi, lakini upande wa serikali ulikuwa haujakamilisha kuandika maelezo hayo.

Mweyekiti wa Shirikisho la vyama vya Wafanyabiashara nchini, Bw. Jonson Minja (aliyevaa koti jeusi) huku akiongea na katibu wake Mchungaji Kiondo

Mwendesha mashtaka mwandamizi wa serikali, Rose Shio aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilifika mahakamani hapo leo kwa ajili ya kusikilizwaji wa awali lakini upande wa serikali ulikuwa bado haujakamilisha kuandika maelezo hayo ya awali.

Amesema kuwa kesi hiyo leo imekuja mahakamani kwa ajili ya usikilizwaji wa awali lakini kwa bahati mbaya upande wa serikali umeshindwa kuandika maelezo ya awali kwa hiyo akaomba ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali ya kesi hiyo.

Wakili wa mshtakiwa huyo Godfrey Wasonga amesema hana kipingamizi na ombi hilo la mwendesha mashtaka wa serikali na kuomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

Baada ya maelezo hayo, hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Dodoma, Rhoda Ngimilanga alisema kesi hiyo itatajwa tena Mei 7 mwaka huu na mshtakiwa ameendelea kuwa nje kwa dhamana.