Jumanne , 4th Jun , 2024

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Emmanuel Nchimbi ameanza ziara ya siku tatu mkoani Kilimanjaro katika Jimbo la Hai ambako ndiko Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe anakotokea.

Dkt. Emmanuel Nchimbi, Akiwasili Mkoani Kilimanjaro

Hayo yanajiri ikiwa ni mwezi mmoja baada ya maandamano ya upinzani mkoani Kilimanjaro kufanyika yakiongozwa na Mwenyekiti huyo wa Upinzani, aliyewataka watanzania kupigania haki zao wenyewe.

Dkt. Nchimbi akitokea mkoani Arusha amepokelewa eneo la King'ori na Kamati ya Siasa ya mkoa wa Kilimanjaro ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoani hapo Komredi Patrick Boisafi, ambapo amesifia utendaji kazi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda namna anavyozishughulikia kero na changamoto za wananchi wa Mkoa huo.

Katibu huyo Mkuu aliyepokea mikoba kutoka kwa Daniel Chongolo amefanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Bomang'ombe huku akisisitiza ulazima wa Chama hicho kuendelea kutekeleza ilani yao ya 2020-2025.

Akiwa mkoani Kilimanjaro atafanya mikutano ya hadhara katika majimbo ya Moshi Mjini, Mwanga na Same Kisha kuendelea na ziara yake mkoani Tanga.

Jimbo la Hai limekuwa ni ngome ngumu kwa CCM licha ya wakati wa serikali ya awamu ya Tano  kuchukuliwa na Mbunge wa Sasa wa chama hicho Mafue Saashisha wa CCM kushika hatamu za uongozi.