Jumatatu , 29th Dec , 2014

Mh. Stephen Wassira, amekiri kuwa kutochukua hatua za mapema kuhusu sakata la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow ni moja ya sababu ambayo imesababisha chama hicho kutofanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi CCM, Mh Stephen Wassira.

Mh,Wassira ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu ameyasema hayo nyumbani kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Kijijini Butiama, ambapo amesema kitendo cha serikali kushindwa kutoa taarifa kwa wakati kimechangia kuwachanganya Watanzania kuhusu sakata hilo.

Hata hivyo mjumbe huyo amesema hivi sasa taifa linakabiliwa na wimbi kubwa la baadhi ya viongozi wake kukosa uzalendo na uadilifu huku wakitanguliza mbele maslahi binafsi kitendo ambacho amesema kinaondoa dhana nzima ya kumuenzi baba wa taifa

Naye mmoja ya watoto wa baba wa Taifa Mh. Makongoro Nyerere, ametumia mazungumza hayo na Mh. Wassira kuitahadharisha CCM, kuwa endapo itashindwa kudhibiti vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi kuna hatari ya kuwagawa watanzania na kufanya CCM kupoteza dola katika uchaguzi mkuu ujao.