Jumatano , 5th Jun , 2024

Serikali imetajwa kwamba itatekeleza kwa asilimia 20 kazi zote za urasimishaji mijini kupitia mradi wa uboreshaji usalama wa milki za ardhi (LTIP) kupitia watumishi walioko katika halmashauri husika na asilimia 80 ya kazi hiyo zitatekelezwa na makampuni binafsi yaliyosajiliwa kufanya kazi

za upangaji (mipango miji) na upimaji wa ardhi.

Hayo yamebainishwa na mwakilishi wa Meneja Urasimishaji Mjini katika mradi huo Paul Kitosi wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri ya wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro

Imebainishwa kuwa katika Halmashauri ya wilaya ya Moshi mradi umepanga kutoa hati 32,000 katika Kata 9 ambapo kazi hiyo itafanywa na makampuni binafsi na tayari kazi hiyo imetangazwa kupitia mfumo wa manunuzi ambapo wataalamu washauri wanaojishughulisha na masuala ya mipango miji na upimaji wanatakiwa kuomba kabla ya tarehe 7 Juni 2024.

Nae Katibu Tawala wa wilaya ya Moshi Shaban Mchomvu kwa niaba ya Mkuu wa wilaya amesema kuwa wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi huo na kuahidi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wake hasa kwa kuzingatia haki za makundi maalumu.