Alhamisi , 24th Jul , 2014

Sakata la mabaki ya viungo vya binadamu kukutwa yametupwa Bunju A nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, limechukua sura mpya baada ya Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuunda kamati maalumu ya watu 15 kuchunguza tukio hilo.

Naibu Waziri wa afya na ustawi wa Jamii nchini Tanzania, Dkt Kebwe Stephen Kebwe (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na waziri wa wizara hiyo Dkt Seif Rashid.

Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Kebwe Steven Kebwe ametangaza hatua hiyo leo Jijini Dar es salaam na kusema kuwa kamati hiyo inahusisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya Vyuo Vikuu, Baraza la Madaktari, Ofisi ya Mkemia Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, pamoja na walalamikiwa ambao ni Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia ( IMTU).

Kwa mujibu wa Dkt Kebwe, kitendo cha kutupa viungo vya binadamu kama ilivyotokea kwa tukio la Bunju A hakikubaliki kwani licha ya kuwa kinyume cha sheria, taratibu na miongozo ya ufundishaji wa taaluma za afya, kinadhalilisha utu na thamani ya mwanadamu.

Aidha katika hatua nyingine, serikali ya Uingereza imetangaza kusitisha utoaji wa vyandarua vya gharama nafuu vinavyotolewa kwa akina mama wajawazito na watoto wadogo nchini kupitia mpango wa hati punguzo, kutokana na kile ilichoeleza kuwa ni kuwepo ufisadi mkubwa ambapo sehemu kubwa ya vyandarua hivyo haviwafikii walengwa.

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Kebwe Stephen Kebwe, amesema hayo leo jijini Dar es salaam na kufafanua kuwa hatua hiyo ya Uingereza inatokana na uchunguzi uliofanywa ambao umeonesha kuwa sehemu kubwa ya vyandarua hivyo vimekuwa vikiishia kwenye maduka binafsi ambako huuzwa kwa bei ya juu.