Alhamisi , 12th Oct , 2023

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) kwa mafanikio makubwa katika kutekeleza afua za VVU na UKIMWI nchini.

Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stanslaus Nyongo, na kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Stanslaus Nyongo wakati kamati ilipofanya ziara ya kutembelea na kukagua mpango wa dreams kupitia mradi wa Epidemic Control (EPIC) unaotekelezwa na Shirika la Family Health International (FHI360) kwa wasichana balehe na wanawake vijana (AGYW) katika katika mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza mara baada ya kukagua vikundi vya vijana  vikiwemo  Sitetereki kilichopo Kata ya Old Shinyanga, Jahazi, Kata ya Ibadakuli na Tunaweza katika Kata ya Kolandoto Mhe. Nyongo amesema lengo la ziara ni kujionea maendeleo ya mradi huo na kuishauri Serikali maeneo ya kuboresha ili kuendeleza jitihada za kuwa na vijana wenye afya nzuri wanaoshiriki katika shughuli za uzalishaji na kujiletea maendeleo yao.

"Tunapongeza kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kumlinda mtoto wa kike hasa  katika  gonjwa kubwa la  UKIMWI, namna ya kumkomboa mtoto wa kike, kujifunza kazi za ujasiliamali ili kujikwamua katika maisha pamoja kupaza sauti dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia hivyo sisi kama wabunge tumeridhishwa na kazi inayofanywa na Serikali," Amesema Mwenyekiti huyo.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga amewaomba vijana wa kike kuendelea kujiamini na kufanya kazi vizuri kwani serikali ya awamu ya sita inawajali vijana na kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa.