Alhamisi , 18th Dec , 2014

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka serikali kupitia upya na kurekebisha sheria inayounda shirika la reli ya Tanzania na Zambia, TAZARA,

Waziri wa uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe

Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu wameitaka serikali kupitia upya na kurekebisha sheria inayounda shirika la reli ya Tanzania na Zambia, TAZARA, ili shirika hilo lijiendeshe kibiashara na kuwanufaisha watanzania kiuchumi badala ya kuendelea na sheria ya sasa ambayo imepitwa na wakati na kwa kiasi kikubwa inawanufaisha zaidi wazambia.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakiwa wameambatana na waziri wa uchukuzi, Dk. Hurrison Mwakyembe wamesafiri kwa gari moshi kutoka jijini Dar es Salaam hadi Mbeya kisha wakatembelea mgodi wa kusaga kokoto na kiwanda cha mataluma cha Kongolo Mswiswi wilayani Mbarali kabla ya kuelekea kwenye karakana ya kukarabati vichwa vya treni jijini Mbeya ambako wamejionea utajiri mkubwa wa TAZARA usiotumika ipasavyo kuwanufaisha watanzania.

Baada ya ziara hiyo wajumbe hao wakaketi chini kufanya majumuisho na ndipo wajumbe wa kamati hiyo wakaitaka serikali kuipitia upya sheria ya TAZARA ili shirika hilo liweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Juma Kapuya amesema kuwa baada ya kamati yake kutembelea shirika la TAZARA kuanzia Dar es Salaam hadi Mbeya, imejionea mambo mengi ambayo serikali inapaswa kushauriwa, hivyo kamati yake itaketi na kuchambua mambo ya muhimu zaidi kwa ajili ya kuyafikisha rasmi serikalini.

Waziri wa uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa anakubaliana na mapendekezo ya kamati hiyo kwa kuwa sababu za kutungwa kwa sheria ya TAZARA wakati ule hivi sasa hazipo na umefika wakati wa shirika hilo kujiendesha kibiashara.