Jumatano , 27th Aug , 2014

Jukwaa la katiba nchini Tanzania limeitaka serikali kusitisha mara moja mchakato wa kutafuta katiba mpya ikiwemo vikao vya bunge maalum la katiba vinavyoendelea mjini Dodoma, kutokana na kile ilichoeleza kuwa ni kukwama kwa mchakato huo.

Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba nchini Tanzania, Hebron Mwakagenda.

Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bw. Hebron Mwakagenda tamko hilo kutokana na kile alichoeleza kuwa ni ishara dhahiri za kukwama kwa mchakato huo, ambao amesema umekuwa ukitumia kiasi kikubwa cha pesa za walipa kodi licha ya kutokwepo kwa muafaka baina ya pande zinazopingana katika bunge hilo.

Kwa mujibu wa Mwakagenda, kuna haja ya nguvu kubwa kwa sasa zielekezwe katika kujiandaa na uchaguzi mkuu wa rais na wabunge hapo mwakani na kwamba mchakato wa kutafuta katiba mpya uendelee baada ya uchaguzi huo.

Aidha, Mwakagenda ametaja viashiria vya kuvurugika kwa mchakato huo kuwa ni hatua ya sasa ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ya kuanza kukusanya maoni, kazi aliyosema kuwa ilishafanywa na tume ya marekebisho ya katiba iliyokuwa chini ya Jaji Mstaafu Joseph Warioba.