Jumatano , 6th Aug , 2014

Jukwaa la katiba nchini Tanzania limesikitishwa na namna Bunge Maalumu la Katiba linavyotaka kunyamazisha sauti na mijadala ya wananchi, kuhusu kasoro zinazojitokeza katika mchakato unaoendelea wa kutafuta katiba mpya.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba nchini Tanzania, Deus Kibamba.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Bw. Deus Kibamba ametoa kauli hiyo katika mahojiano na East Africa Radio leo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja tangu kuanza kwa vikao vya bunge maalumu la katiba ambapo baadhi ya wajumbe wa bunge hilo wamenukuliwa wakiitaka serikali izuie midahalo ya wazi kuhusu mchakato wa katiba mpya.

Katika siku yake ya kwanza ya awamu ya pili ya vikao vya Bunge Maalumu la Katiba; baadhi ya wajumbe wa bunge hilo wamesikika wakiitaka serikali izuie mijada inayoendelea kuhusu katiba mpya kwa madai kuwa imekuwa ikichochea baadhi ya pande zinazogomea mchakato huo kuendelea na msimamo wa kutotaka kurudi bungeni.

Baadhi ya wajumbe hao wameenda mbali kwa kuvihusisha vyombo vya habari kuwa vimekuwa vikichochea mpasuko huo, dhana ambayo imepingwa vikali na Kibamba ambaye amesema ibara ya kumi na nane ya katiba ya sasa inato fursa na uhuru wa mawazo kwa kila Mtanzania.

Aidha, Kibamba amesema mwishoni mwa wiki hii Baraza la Vyama vya Siasa litakutana na pande hasimu katika mchakato wa katiba, ikiwa ni sehemu ya harakati za kupatanisha pande hizo, katika kile alichoeleza kuwa ni fursa pekee na ya mwisho ya kunusuru mchakato huo dhidi ya hatari ya kuvunjika.

Kibamba amesema hana imani iwapo mazungumzo ya mwishoni mwa wiki yataweza kunasua mchakato huo kwani kuna kila dalili kwamba pande zote hasimu zimeshapoteza misingi muhimu ya kufikia maridhiano katika mchakato wa kutafuta katiba mpya.