Jumamosi , 24th Oct , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli, amewataka viongozi wa serikali na wale ambao watateuliwa kuwa Marais siku zijazo, wahakikishe hawafanyi ubinafsishaji wowote wa mashirika badala yake yabaki kuwa chini ya serikali ili yaweze kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 24, 2020, jijini Arusha wakati wa uzinduzi wa safari za Treni ya kuanzia Dar es Salaam, Tanga, Moshi na Arusha ambayo ilikuwa imesimama kufanya shughuli zake kwa takribani miaka 30, ambapo pia amesisitiza utunzwaji wa miundombinu ya Treni hiyo.

"Niwaombe viongozi wenzangu serikalini hili liwe fundisho tusikubali tena kubinafsisha vitu vya msingi katika nchi, tulibinafsisha Ndege na Treni tukaja kuanza upya, mimi sitakuwa Rais wa maisha lakini natoa ujumbe kwa wale watakaokuja baadaye hili liwe fundisho, hata nchi zilizoendelea mashirika yao hawajayabinafsisha, ibaki kuwa ndani ya serikali na inapokuwa ndani ya seriklai huduma kwa wananchi wanyonge itawafikia", amesema Rais Magufuli

Aidha Rais Magufuli akatoa msisitizo kwa Watanzania juu ya suala la kuaminiana, "Vichwa vya Watanzania vina akili mno lakini tatizo hatuaminiani, ninawaomba kupitia mfano huu wa TRC tuanze kujiamini tutafanya makubwa ambayo wengine hawawezi kuyafanya, mabehewa yote ya mizigo 347 yamekarabatiwa hapa, na 20 ya abiria nayo yamekarabatiwa hapa".