Jumamosi , 3rd Oct , 2020

Mgombea wa urais kupitia CCM, Dkt John Magufuli akiwa Unguja leo, tarehe 3 Oktoba, amewambia maelfu ya waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni kuwa wamchague Dkt. Hussein Mwinyi kwa sababu ambazo amezianinisha katika makundi tofauti zikiwamo za kiutendaji na umri wake.

Mgombea urais kupitia CCM, Dkt John Magufuli.

Magufuli amezitaja sababu hizo wakati akimnadi mgombea wa Urais Visiwani Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Mwinyi, kuwa kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka katika wizara mbalimbali ikiwemo ile ya Ulinzi, kwa kipindi chote alikuwa mwaminifu na asiyekuwa na tamaa hivyo kuwaomba Wazanzibar wamchague kwa kishindo.

''Mh Mwinyi Hussein amekuwa Waziri wa ulinzi miaka 11, mizinga yote inamjua, vifaru vyote vinamjua, helikopita za vita zote zinamjua ,mabomu yote yanamjua miaka 11 iko chini yake, Baba huyu hakuwa na tamaa hata ya kupindua serikali, mtu unavifaru na ndege kila kitu chako si ungeweza hata kupindua serikali ukawa Rais, ana moyo wenye uvumilivu na wa kipekee'', Dkt John Magufuli, mgombea urais CCM.

Aidha ameitaja sababu nyingine kuwa ni umri alionao Mwinyi, kwa sasa unashabihiana na idadi kubwa ya Wazanzibari ambao wamezaliwa baada ya Muungano huku wakiwa ndiyo idadi kubwa ya wapiga kura na watu ambao wanahitaji mabadiliko na maendeleo.

''Tangu Muungano wetu uanzishwe Marais wote walioiongoza Zanzibar wamekuwa ni wale waliozaliwa kabla ya Muungano, safari hii CCM imeamua kumleta kijana aliyezaliwa baada ya Muungano ambaye ni Hussein Mwinyi na hii inaendana na hali halisi ya Zanzibar hivi sasa takribani 70% ya Wazanzibar wamezaliwa baada ya Muungano kwa hiyo yeye ni mtu sahihi'', ameongeza.