Jumanne , 6th Dec , 2016

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwakaribisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo aliyeambatana na Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe kabla ya kuanza kwa kikao chao cha pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan

Rais Magufuli amesema badala ya kufukuzwa, wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake aondolewe.

"Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu".

"Na hizi ndio ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda kuwafukuza watu 5,000? haiwezekani na wala haingii akilini" amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo kwa kutengeneza nyaraka zinaonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.

Hata hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa Wamachinga na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria bali wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge