Jumanne , 10th Jan , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Nigeria Profesa Ibrahim Gambari nyumbani kwake Chato Mkoani Geita.

Rais Magufuli akipokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Nigeria kupitioa kwa Prof. Ibrahim Gambari

Mazungumzo yao yalilenga masuala mbalimbali ya uhusiano kati ya Tanzania na Nigeria.

Rais Dkt. Magufuli amempongeza Rais Muhammadu Buhari kwa jitihada kubwa anazochukua kwa ajili ya kuleta maendeleo nchini mwake.

Pia, Rais Dkt. Magufuli amempongeza Rais Buhari kwa jitihada anazozifanya za kukabiliana na kundi la Boko Haram ili kuhakikisha amani inaendelea kudumu nchini mwake.

Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari

Kwa upande wake Mjumbe Maalum wa Rais wa Nigeria, Profesa Ibrahim Gambari amempongeza Rais Dkt. Magufuli kwa ushindi alioupata na jitihada anazochukua katika kupambana na rushwa na kubana matumizi jambo ambalo linaungwa mkono na wananchi wengi wa Nigeria.

Profesa Gambari alimkabidhi Rais Dkt. Magufuli barua yenye ujumbe maalum kutoka kwa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria.