Alhamisi , 25th Dec , 2014

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ametakiwa kutowaonea aibu mawaziri wasiotimiza majukumu yao katika kuwatumikia wananchi badala yake awachukulie hatua za haraka za kuwawajibisha.

Waumini wa madhehebu mbalimbali ya kikristo nchini Tanzania leo wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha siku kuu ya Krismas ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Kwa hapa Tanzania ibada ya kitaifa imefanyika katika kanisa la pamoja la jumuiya ya Kikristo Chuo Kikuu cha Dar es salaam na kuongozwa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Askofu Henry Hafidh.

Katika mahubiri yake Askofu Hafidh amemtaka Rais Kikwete kutowafumbia macho mawaziri wazembe na wale wasiotimiza majukumu yao katika kuwatumikia watanzania.

Pia amewataka waandishi wa Habari nchini kutumia kalamu zao kwa kuandika mambo mema kwa nchi na yenye kuleta tija kwa kwa maendeleo ya taifa na si kuandika habari ambazo zitavuruga amani ya nchi.

Ameongeza kuwa waandishi ndio wana jukumu la kuwabadilisha wananchi kupenda habari njema kuliko hivi sasa ambapo wanashabikia habari zenye dalili ya kutaka kuvunja amani ya nchi.

Aidha Askofu Hafidh ameonya viongozi wa dini kuacha kushabikia masuala ya siasa ambayo inawaingiza kwenye mapambano ya wenyewe na kuacha kufanya kazi ambayo wameagizwa na mwenyezimungu juu ya wana damu.

Amesema wanapoona viongozi wa kisiasa wanakosea, jukumu lao ni kupiga magoti na kuwaombea badala ya kuingilia mambo yasiyowahusu.