Jumamosi , 17th Feb , 2018

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa amesema wamefanikiwa kupata taarifa katika mtandao za mtu anayehamasisha vijana wa CUF kujitokeza kufanya vurugu kwenye vituo.

Kamanda Mambosasa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza mubashara akiwa katika Jimbo la Kinondoni juu ya hali ya kiusalama na kusema hawajapata changamoto ya aina yeyote za kiharifu au waharifu.

"Kwa ujumla hali ya vituo vyote vya kupigia kura 610 vya Jimbo la Kinondoni vipo salama kabisa, hatujapata changamoto yeyote za kiharifu wala waharifu. Tunaendelea kusimamia upigaji kura", amesema Kamanda Mambosasa.

Pamoja na hayo, Kamanda Mambosasa ameendelea kwa kusema "nitoe onyo tu kwa wananchi, tunazo taarifa za mtu aliyeanzisha kwenye mtandao za kuwataka vijana wa chama cha CUF wajikusanye kuja kufanya fujo wakati wa kuhesabu au kutangaza matokeo. Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu yeyote ambae atajaribu kuvuruga uchaguzi huu ambao kimsingi tunakwenda kumaliza salama".

Kwa upande mwingine, zoezi la kupiga kura sasa limekwisha fungwa kwa wananchi kulingana na sheria za Tume ya Uchaguzi ambako sasa wasimamizi wa vituo kwa kushirikiana na mawakala wa vyama mbalimbali wameanza kuhesabu kura zilizopigwa.