Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekamata vipande 156 vya meno ya tembo ambayo ni sawa na tembo wapatao 45, nyara hizo zimekamatwa eneo la Temeke Sudan ambapo jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa Robert Isaac na Salum Aiyo Mnekeya waliokutwa na nyara hizo za serikali.
Akiongea leo jijini Dar es Salaam Kamanda wa Kanda Maalumu ya mkoa wa Dar es Salaam Kamishna Suleiman Kova amesema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na ushirikiano wa wananchi waliotoa taarifa polisi.
Kuhusu suala la watuhumiwa wa makontena yaliyopotea katika bandari ya Dar es salaam Kamanda Kova amesema wataendelea na operesheni hiyo. Kamanda Kova pia ametoa taarifa kuwa tayari jeshi hilo limejipanga kudhibiti uhalifu jijini Dar es salaam wakati huu wa sikukuu za, Maulid, Krismasi na mwaka mpya.