Jumatano , 8th Jan , 2020

Familia za watu sita wanaoishi katika nyumba za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), zilizopo katika eneo la Isamilo mkoani Mwanza, wamenusurika kifo baada ya moto uliozuka katika jengo hilo na kuteketeza mali zote.

Jengo likiteketea kwa moto.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto mkoani Mwanza, Kamishna Mwandamizi, Ambwene Mwakibete, amesema jeshi lake lilifanikiwa kuuzima moto huo, japo walikuta tayari mali za familia hizo zikiwa zimeshateketea, huku Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi, ACP Safia Jongo, akisema mbali na mali chache kuokolewa hakuna mtu aliyepoteza maisha katika ajali hiyo ya moto.

"Bahati mbaya TANESCO walichelewa kufika na kwasababu ni majengo na umeme ulikuwa bado haujakatwa, ule umeme ukaanza kurudi kwenye gari na kupelekea hali hatarishi kwenye gari la zimamoto, kwahiyo ikabidi kusubiria hadi wao wafike lakini baadae walifika na kwa pamoja tukashirikiana kuudhibiti huu moto" amesema Kamanda wa Jeshi la Zimamoto, Mwakibete.

Tukio hilo limetokea jana Januari 8, 2020, majira ya saa 1:00 jioni, ukitokea katika ghorofa ya pili ya jengo hilo, lililopo mtaa wa Nyakabungo B, eneo la Isamilo kitalu namba 81 wilayani Nyamagana, uliteketeza mali zote za familia sita huku ukiziacha familia hizo katika hali ya sintofahamu.