Kufuatia kupatikana na hatia ya kuwa na nyara za Serikali na kumiliki silaha isivyo halali, watuhumiwa Idd Hamis Mohamed (55) na Huruma Mlengule Hosia (35), wakazi wa Kijiji cha Mseko wamehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga, mnamo Novemba 14, 2025 cha miaka 25 kila mmoja.
Inadaiwa kuwa mnamo Januari 5, 2025 katika eneo la Msubugo, Kijiji cha Mseko, Kata ya Kipumbwi, Tarafa ya Mwera, watuhumiwa walikamatwa na Askari Polisi wakishirikiana na Askari wa Uhifadhi ya Taifa Saadani wakiwa na nyama ya digidigi watatu yenye thamani ya Tsh 2,214,810, pamoja na silaha aina ya gobole.
Baada ya kukamatwa, kesi ilifunguliwa katika Kituo cha Polisi Pangani siku hiyo hiyo na upelelezi ukaanza mara moja. Upelelezi ulipokamilika tarehe 20 Mei, 2025, watuhumiwa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Pangani, ambapo shauri lilipewa namba 372/2025 na kupelekwa mbele ya Mheshimiwa Hakimu Husna Mwiula – SRM.
Licha ya watuhumiwa kukana mashtaka yao mara baada ya kusomewa, shauri liliendelea kwa kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na watuhumiwa wote wawili kupatikana na hatia, iliwapa hukumu ya kifungo cha kutumikia miaka 20 gerezani kwa kosa la kupatikana na nyara za Serikali na kifungo cha miaka 5 gerezani kwa kosa la kumiliki silaha isivyo halali.
