Pia, imezielekeza taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2025.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali inazihimiza taasisi hizo kwa sasa kutumia nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia.
Waziri Jafo amesema watumiaji wakubwa wa nishati za kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni taasisi za umma na binafsi, hivyo kutokana na athari zake kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi, Serikali imeandaa Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.
Aidha, Jafo amesema kuwa Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2019 inaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya kuni na mkaa.
Waziri Jafo amefafanua kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kutokana na watu wengi kufanya shughuli zisizo endelevu ikiwemo kutumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia kutokana na nishati hiyo kupatikana kwa urahisi na watu wengi wanaweza kumudu gharama yake.
Akifafanua zaidi Dkt. Jafo amesema kutokana na athari hizo zilizojitokeza, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga uchumi wa viwanda, hivyo matumizi ya nishati mbadala ikiwemo mkaa mbadala yatatoa fursa ya viwanda vya kutengeneza mkaa mbadala sanjari na kuzalisha majiko sanifu na banifu kwa ajili ya matumizi fanisi ya nishati hiyo.







