Ijumaa , 1st Mei , 2020

Mwili wa aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Jaji Augustino Ramadhani umeagwa rasmi kitaifa leo Ijumaa Mei Mosi, 2020, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam.

Jeneza lenye Mwili wa Marehemu Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Jaji Augustino Ramadhani.

Akiongea wakati wa kuaga, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma, amesema kama wanataaluma wa sheria watafanya kumbukumbu ya kumuaga kitaaluma kwasababu wameshindwa kufanya hivyo sasa kutokana na janga la Corona.

Aidha ameeleza utumishi wa Jaji Ramadhani kwa taifa kama kitu cha kukumbukwa zaidi hasa alivyoweza kutumika kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Jeshi, sheria, dini na michezo, huku akiiwakilisha nchi kwa kuwa Rais wa Mahakama ya Afrika.

''Jaji Augustino Ramadhani alikuwa Rais wa kwanza wa wa Shirikisho la mchezo wa Kikapu nchini (TBF) na mpaka anafariki alikuwa ni mlezi wa shirikisho hilo, hivyo atakumbukwa zaidi kwa jinsi alivyolitumikia taifa kwenye michezo ndani na kimataifa'' - Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma.

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi ambaye aliiwakilisha serikali amesema ''Marehemu Jaji Augustino Ramadhani alikuwa na kipawa cha aina yake katika uongozi na taifa litamkumbuka siku zote na kwa niaba ya Serikali, natoa pole kwa mke wa marehemu, watoto pamoja na ndugu wote''.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi akiongea wakati wa kuaga

Hafla hiyo ya kuagwa kwa marehemu Jaji Ramadhani imehudhuriwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mh. Benjamin Mkapa na Rais mstaafu wa awwamu ya nne Mh. Jakaya Kikwete.