Alhamisi , 17th Jul , 2014

Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande amesema Katiba mpya itapatikana aendapo kutakuwepo na makubaliano baina ya wajumbe wa bunge la Katiba ambao wanaounganishwa na vyama vya siasa na taasisi mbalimbali nchini.

Jaji mkuu wa Tanzania mheshimiwa Othman Chande.

Jaji chande amesema hayo jana Jijini Dar es Salaam baada ya mkutano baina ya Tume ya Utumishi wa mahakama ya Uganda na ya Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa tume hizo katika utendaji ili kuweza kupata utaratibu wa namna ya uteuzi wa majaji na Jaji Mkuu katika mahakama nchini Tanzania.

Aidha Jaji Chande ameeleza Katiba ni chombo cha kugawa madaraka na kuwa chimbuko la kujenga na kukuza muafaka, ambapo amesema njia kuu ya kupata Katiba mpya ni kupitia makubaliano baina ya wananchi wa nchi husika.

Wakati huo huo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC) kipo hatarini kufungwa na shughuli zake kusitishwa moja kwa moja, iwapo Mahakama Kuu nchini itaruhusu tozo ya fedha ya shilingi bilioni 2.8 ambazo kituo hicho kinatakiwa kuilipa kampuni ya kufua umeme ya Dowans.

Iwapo hatua hiyo itatekelezwa, itakuwa na athari kubwa kwa zaidi ya Watanzania 15,000 ambao baadhi yao kituo hicho kinawatetea katika mashauri ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyofunguliwa kwenye mahakama mbali mbali nchini na ambayo yanaendelea katika mahakama hizo.

Akizungumza katika mahojiano na EATV jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo hicho Dkt. Helen Kijjo—Bisimba, ameitafsiri tozo hiyo kama njama za chini kwa chini za kutaka kukifuta kituo hicho, kwani mazingira ya namna ilivyopata baraka na kusajiliwa na mahakama yanatia shaka kwa madai ya LHRC kutoshirikishwa.

Aidha, tofauti na inavyodhaniwa na wengi kwamba kituo hicho kimekuwa kikipingana na serikali, Dkt Kijo-Bisimba amesema LHRC imekuwa msaada kwa jamii na hata kwa serikali yenyewe na kutolea mfano namna wanasheria wa kituo hicho, walivyochangia ushindi wa serikali katika kesi baina yake na iliyokuwa kampuni ya kusambaza maji jijini Dar es Salaam ya Bywater, kesi iliyofunguliwa katika mahakama ya kimataifa ya migogoro ya kibishara.